Matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi: mfano wa shule za upili za kaunti ndogo ya Moiben, Kenya
Loading...
Date
2019-11
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
KIBU
Abstract
Utafiti ulichunguza matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa
sarufi katika shule za upili zilizoko kaunti ndogo ya Moiben. Malengo ya utafiti yalikuwa
ni: Kuthibitisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa, kuchunguza jinsi walimu hutumia vifaa
vya kisasa katika kufundisha sarufi, kuhakiki umuhimu wa matumizi ya vifaa vya kisasa
katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Utafiti ulifanyika katika kaunti ndogo ya
Moiben iliyoko katika kaunti ya Uasin Gishu. Eneo hili lilichaguliwa kimakusudi
kuwakilisha maeneo mengine nchini Kenya yenye sifa sawa za ufundishaji na ujifunzaji.
Utafiti uliongozwa na nadharia ya kujifunza kiugunduzi yake Bruner (1966). Utafiti
ulizingatia muundo wa utafiti kimfano. Ulilenga shule za upili kumi na tano kati ya
ishirini na sita zilizoko katika kaunti ndogo ya Moiben. Walengwa walikuwa walimu
kumi na watano wanaofundisha sarufi na wanafunzi mia moja na watano wa kidato cha
tatu. Walimu walichaguliwa kwa kuzingatia vipindi vya sarufi ya Kiswahili
wanavyovifundisha. Wanafunzi wa kidato cha tatu walihusishwa kwa kuwa mada
zilizolengwa katika utafiti zilifundishwa katika kidato cha tatu. Hojaji, mahojiano na
uchunzaji zilitumika kukusanya data. Uchunzaji ulitumika kupata data kuhusu vifaa
vinavyotumika darasani kufundisha sarufi. Hojaji ya mwalimu na mwanafunzi ilitumika
kupata data kuhusu umuhimu wa matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na
ujifunzaji wa sarufi. Mahojiano yalitumika kupata data kuhusu changamoto za matumizi
ya vifaa vya kisasa. Data iliyokusanywa iliwasilishwa kwa kutumia asilimia majedwali.
Hatimaye, data hii ilichanganuliwa kimaelezo. Matokeo ya utafiti yalibaini kuwa, chini
ya asilimia 20 ya walimu katika kaunti ndogo ya Moiben walitumia tarakilishi na
vipakatalishi pamoja na vinuruweo katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Matokeo
yalithibitisha kuwa, vifaa hivi hurahisisha uelewekaji wa mada za sarufi, huleta
uchangamfu darasani, huokoa muda na kuwashirikisha wanafunzi katika somo. Matumizi
ya vifaa hivi yanakumbwa na changamoto kama vile: ukosefu wa mtandao shuleni, idadi
kubwa ya wanafunzi, hitilafu za umeme, upungufu wa fedha za kuvinunua vifaa hivi,
upungufu wa wakati na upungufu wa ujuzi wa matumizi baina ya walimu. Matokeo ya
utafiti huu yatakuwa ya manufaa kwa wizara ya Elimu nchini Kenya. Kutokana na
changamoto zinazokumba matumizi ya vifaa vya kisasa, matokeo haya yanaweza
yakaisaidia Wizara ya Elimu kubuni mikakati ya kuzikabili changamoto hizi na
kuyaboresha matumizi ya vifaa hivi. Aidha, yatawanufaisha walimu wa shule za upili
kwa kuwa yatatoa fahamu zaidi kuhusu matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji
na ujifunzaji wa sarufi.