Department of Kiswahili and Other African Languages

Permanent URI for this collectionhttp://erepository.kibu.ac.ke/handle/123456789/161

Browse

Recent Submissions

Now showing 1 - 5 of 5
  • Item
    Matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi: mfano wa shule za upili za kaunti ndogo ya Moiben, Kenya
    (KIBU, 2019-11) Joachim, Melly Kipchirchir
    Utafiti ulichunguza matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi katika shule za upili zilizoko kaunti ndogo ya Moiben. Malengo ya utafiti yalikuwa ni: Kuthibitisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa, kuchunguza jinsi walimu hutumia vifaa vya kisasa katika kufundisha sarufi, kuhakiki umuhimu wa matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Utafiti ulifanyika katika kaunti ndogo ya Moiben iliyoko katika kaunti ya Uasin Gishu. Eneo hili lilichaguliwa kimakusudi kuwakilisha maeneo mengine nchini Kenya yenye sifa sawa za ufundishaji na ujifunzaji. Utafiti uliongozwa na nadharia ya kujifunza kiugunduzi yake Bruner (1966). Utafiti ulizingatia muundo wa utafiti kimfano. Ulilenga shule za upili kumi na tano kati ya ishirini na sita zilizoko katika kaunti ndogo ya Moiben. Walengwa walikuwa walimu kumi na watano wanaofundisha sarufi na wanafunzi mia moja na watano wa kidato cha tatu. Walimu walichaguliwa kwa kuzingatia vipindi vya sarufi ya Kiswahili wanavyovifundisha. Wanafunzi wa kidato cha tatu walihusishwa kwa kuwa mada zilizolengwa katika utafiti zilifundishwa katika kidato cha tatu. Hojaji, mahojiano na uchunzaji zilitumika kukusanya data. Uchunzaji ulitumika kupata data kuhusu vifaa vinavyotumika darasani kufundisha sarufi. Hojaji ya mwalimu na mwanafunzi ilitumika kupata data kuhusu umuhimu wa matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Mahojiano yalitumika kupata data kuhusu changamoto za matumizi ya vifaa vya kisasa. Data iliyokusanywa iliwasilishwa kwa kutumia asilimia majedwali. Hatimaye, data hii ilichanganuliwa kimaelezo. Matokeo ya utafiti yalibaini kuwa, chini ya asilimia 20 ya walimu katika kaunti ndogo ya Moiben walitumia tarakilishi na vipakatalishi pamoja na vinuruweo katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi. Matokeo yalithibitisha kuwa, vifaa hivi hurahisisha uelewekaji wa mada za sarufi, huleta uchangamfu darasani, huokoa muda na kuwashirikisha wanafunzi katika somo. Matumizi ya vifaa hivi yanakumbwa na changamoto kama vile: ukosefu wa mtandao shuleni, idadi kubwa ya wanafunzi, hitilafu za umeme, upungufu wa fedha za kuvinunua vifaa hivi, upungufu wa wakati na upungufu wa ujuzi wa matumizi baina ya walimu. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa ya manufaa kwa wizara ya Elimu nchini Kenya. Kutokana na changamoto zinazokumba matumizi ya vifaa vya kisasa, matokeo haya yanaweza yakaisaidia Wizara ya Elimu kubuni mikakati ya kuzikabili changamoto hizi na kuyaboresha matumizi ya vifaa hivi. Aidha, yatawanufaisha walimu wa shule za upili kwa kuwa yatatoa fahamu zaidi kuhusu matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi.
  • Item
    Mchango wa tamasha za muziki katika ufundishaji wa uainishaji wa nyimbo katika shule za upili nchini kenya
    (KIBU, 2019-11) Angushi, Magambo Emilly
    Wizara ya Elimu imekuwa ikitumia tamasha za muziki kuwaelimisha wanafunzi na hadhira kuhusu masuala mbalimbali. Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu kipera cha nyimbo, lakini kuna haja ya kuchunguza njia mbadala za ufundishaji wa kipera cha nyimbo kwa sababu ni kipana mno na hata uainishaji wake hukanganya. Utafiti huu ulichunguza mchango wa tamasha za muziki kwa ufundishaji wa uainishaji wa nyimbo katika shule za upili nchini Kenya. Malengo mahususi ya utafiti huu yalikuwa: kupambanua uainishaji wa nyimbo katika tamasha za muziki, kubainisha namna uainishaji huu unavyoweza kutumiwa kufundisha uainishaji wa nyimbo darasani na kudhihirisha dhima ya nyimbo kupitia tamasha za muziki. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya utanzu, mhimili wa pili unaosema kuwa, tanzu huleta muwala katika matini na kufanya kazi ieleweke kwa urahisi, pamoja na nadharia ya ujifunzaji kijamii, mhimili wa tatu unaoshadidia kuwa ujifunzaji hushirikisha utazamaji. Sampuli iliyolengwa katika utafiti huu ilijumuisha shule zilizoshiriki katika mashindano ya tamasha za muziki ya Kanda la Magharibi zilizofanyika mwaka wa 2018. Utafiti huu ulifanywa kwenye mashindano ya tamasha za muziki kiwango cha kikanda eneo la Magharibi yaliyofanyika katika shule ya upili ya wavulana ya Chavakali iliyo katika Kaunti ya Vihiga ambayo kauli mbiu yake ilikuwa “Kuboresha umoja wa nchi, utangamano na uelewano kupitia tamasha za muziki nchini Kenya.” jambo ambalo lilijitokeza katika uchanganuzi wa data ya utafiti huu hasa kupitia lengo la tatu lililoshughulikia dhima ya nyimbo kupitia tamasha za muziki. Watafitiwa ishirini na tano walihojiwa; wanafunzi 20 na walimu 5 walioteuliwa kinasibu. Mbinu ya kuteua sampuli ilikuwa ya kinasibu. Mbinu hii ya kinasibu ilitumiwa katika kuteua nyimbo 10 zilizotumika katika utafiti huu. Mtafiti alitumia utazamaji na mahojiano kama mbinu za kukusanya data. Data ilikuwa ya kithamano. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kutumia maelezo ya kiufafanuzi na kuwasilishwa kwa maandishi yaliyoambatana na mifano ya nyimbo na picha. Utafiti ulibaini kwamba nyimbo zimeainishwa katika madaraja mbalimbali kutegemea vigezo kama vile umri, mahali na maudhui. Utafiti huu ulidhihirisha kuwa tamasha za muziki zinaweza kuwa njia mbadala ya kufundishia uainishaji wa kipera cha nyimbo katika shule za upili nchini Kenya. Utafiti huu unapendekeza tamasha za muziki zichukuliwe kama mbinu nyingineyo ya kufundishia fasihi simulizi katika shule za upili. Umuhimu wa utafiti huu ni kuwa matokeo yake yataweza kuwafaidi wanafunzi na walimu katika ujifunzaji na ufundishaji wa uainishaji wa nyimbo kama kipera cha fasihi simulizi tunapotilia maanani mtaala mpya unaohimiza umuhimu wa kuendeleza ujuzi na maarifa na pia kuzingatia maarifa hayo katika hali halisi za maisha.
  • Item
    Ufundishaji wa ushairi kwa kutumia tamthilia katika shule za upili nchini kenya: uchunguzi kifani wa kaunti ndogo ya teso kaskazini
    (KIBU, 2019-11) Mukoya, Hillary Mauka
    Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu utanzu mmoja kutumika kuwasilisha mawazo katika utanzu mwingine. Mbinu ya mwelekeo mseto imetafitiwa na wataalam mbalimbali kuhusu isimu kutumika kufundisha fasihi na fasihi kutumika kufundisha isimu. Hata hivyo, mtafiti hajakumbana na utafiti unaohusu utanzu mmoja wa fasihi kutumika kufundisha utanzu mwingine wa fasihi, hasa tamthilia kufundisha ushairi. Kumbe dhana ya usetaji inaweza kutumika katika ufundishaji wa tanzu za fasihi. Kwa hivyo, kuna haja ya kufanya utafiti kuhusu ufundishaji wa ushairi kwa kutumia tamthilia. Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kuchunguza namna tamthilia inavyotumika kufundisha ushairi katika shule za upili zilizoko Kaunti Ndogo ya Teso Kaskazini, Busia Kenya. Malengo mahususi ya utafiti yalikuwa: kuchunguza namna ushairi unavyofundishwa katika shule za upili, kupambanua namna tamthilia inavyoweza kutumika kufundisha ushairi na kueleza mchango wa matumizi ya tamthilia katika ufundishaji wa ushairi. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya utanzu ambayo iliasisiwa na Boas (1940) na kuendelezwa naye Bakhtin (1981). Nadharia hii ina mihimili ifuatayo: Mhimili wa kwanza unaoshikilia kuwa, tanzu huibua muundo wa kazi fulani ya fasihi na kufanya kazi hiyo ieleweke kwa urahisi sana; mhimili wa pili unaeleza kuwa, matumizi ya utanzu mwingine huwafanya wasomaji au wapokezi kuwa na ilhamu zaidi kuliko kuwapa kila wanachotarajia na mhimili wa tatu unashikilia kuwa, tanzu mbili zilizozoeleka zitumike kwa pamoja kwa sababu ya sifa zenye uhusiano mkubwa. Utafiti huu ulitumia muundo wa kimaelezo. Sampuli ya utabakishaji wa kimakusudi ilitumika kuchagua shule za upili tisa (9) zilizowakilisha asilimia thelathini (30%) ya shule zilizo katika Kaunti Ndogo ya Teso Kaskazini iliyo na jumla ya shule thelathini (30). Kwa upande mwingine, sampuli ya kimakusudi ilitumika kuchagua mwalimu mmoja kutoka katika kila shule aliyeshiriki katika utafiti huu. Mbinu za ukusanyaji data zilizotumika ni usaili na uchunzaji. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia malengo mahususi ya utafiti. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa, vipengee vya mtindo, muundo na maudhui katika ushairi vilifundishwa kwa kutumia mbinu tofautitofauti za ufundishaji. Aidha, ilibainika kuwa, tamthilia ya Kifo Kisimani, Mstahiki Meya na Kigogo zilikuwa katika nafasi nzuri ya kufundishia mtindo, muundo na maudhui kwa sababu zilikuwa na bahari mbalimbali za ushairi. Mchango wa matumizi ya tamthilia katika ufundishaji wa ushairi ulionyeshwa; utafiti ulibaini kuwa, ufundishaji wa tamathali za usemi ulifanywa kwa urahisi, muundo wa ushairi ulifafanuliwa vizuri, wanafunzi walielewa maudhui kwa urahisi, walimu walikamilisha silabasi mapema, wanafunzi walichangamkia somo, ilhamu ya kutafiti iliibuliwa miongoni mwa wanafunzi na wanafunzi walimakinika darasani. Utafiti huu unapendekeza kuwa, walimu watilie maanani mbinu mahususi za ufundishaji wanapofundisha vipengee vya ushairi kama vile mtindo, muundo na maudhui ili kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanafurahia utanzu wa ushairi. Vilevile, unapendekeza kuwa, usetaji katika ufundishaji na ujifunzaji uweze kutiliwa maanani na walimu wanapofunza ushairi wa Kiswahili kwa kusudi la kuondoa uchovu miongoni mwa wanafunzi. Aidha, unapendekeza walimu waboreshe mwelekeo wa ufundishaji mseto kusudi mada zinazofundishwa zieleweke bora zaidi. Pia unapendekeza kwamba, walimu wazingatie mchango wa matumizi ya tamthilia katika ufundishaji wa ushairi. Utafiti huu utawasaidia walimu wa shule za upili kuboresha zaidi ufundishaji wa ushairi kwa kuzingatia mbinu mahususi za ufundishaji wa ushairi. Utafiti huu pia utabainisha mchango wa kutumia tamthilia katika ufundishaji wa ushairi na hivyo basi, kufaa asasi zinazowaandaa walimu katika matumizi ya mbinu ya mwelekeo mseto katika ufundishaji wa fasihi.
  • Item
    Tathmini ya vitabu vya kiada katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi ya Kiswahili katika shule za msingi za kaunti ya Busia
    (KIBU, 2018-04) Abai, Rose Ajuma
    Vitabu vya kiada ni nyenzo kuu hasa katika mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji. Ni vigumu kuafikia malengo ya elimu bila vitabu vya kiada. Ni muhimu kuteua kitabu cha kiada kinachofaa.Ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi ya Kiswahili kama msingi wa kukuza lugha ni jambo gumu linalohitaji kutiliwa maanani. Utafiti huu ulipata msukumo kutokana na hali kwamba vitabu mbalimbali vya kiada vimeidhinishwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala Nchini Kenya kwa mitindo tofauti tofauti, kwa utaratibu wa sasa wa biashara huria ya vitabu na ubinafsishaji. Somo moja huweza kuwa na vitabu kadhaa. Ni kwa misingi hiyo ndipo utafiti huu ulidhamiria kutathmini vitabu vitatu vya kiada katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi ya Kiswahili kwa shule za msingi katika kaunti dogo ya Teso Kaskazini Kaunti ya Busia. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kubainisha athari za matumizi ya vitabu vya kiada aina aina katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi ya Kiswahili, kisha kuchanganua mitazamo tofauti ya waandishi katika kueleza vipengele vya sarufi na kupambanua Nguvu Udhaifu Nafasi na Tishio (NGUNATI) ya vitabu vya kiada vya wanafunzi katika ufundishaji wa sarufi ya Kiswahili. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Masharti ya Ujifunzaji. Nadharia hii inasisitiza kushirikishwa kwa michakato ndani ya akili ya binadamu katika kufanikisha ujifunzaji. Muundo wa kimaelezo na kitakwimu na mkabala wa usoroveya ulitumiwa. Umma lengwa ya utafiti huu ilikuwa shule ishirini na nane (28) za msingi zilizoteuliwa kutumia mbinu ya kishada kutoka kwa jumla ya shule themanini na saba (87) zinazopatikana katika kaunti dogo la Teso Kaskazini. Jumla ya walimu ishirini na nane (28) wa somo la Kiswahili waliteuliwa kutumia mbinu ya kimaksudi na wanafunzi mia tatu arobaini na nne (344) waliteuliwa kutumia mbinu ya kinasibu. Jumla ya wasailiwa walikuwa 372. Data katika utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia hojaji na uchanganuzi wa yaliyomo katika vitabu vitatu vya kiada vya Kiswahili. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kutumia majedwali na asilimia. Data iliwasilishwa kwa kupitia maelezo ya kifafanuzi na mifano. Utafiti umebainisha kuwa walimu hutumia kitabu kimoja cha kiada. Kimsingi matokeo ya utafiti huu yamebainisha kuwa, kuna haja ya kutathmini na kufanya marekebisho katika vitabu vya kiada vinavyotumika katika ufundishaji na ujifunzaji wa sarufi ili mahitaji ya wanafunzi yaweze kuafikiwa. Utafiti huu una mchango katika kuelewa uhalisia kuhusu vitabu vya kiada vinavyotumiwa katika shule nchini Kenya. Aidha, matokeo haya yanatarajiwa kuwapa washika dau mfumo wa kinadharia katika kutathmini vitabu vya kiada vinavyofaa kutumiwa katika ufundishaji wa sarufi ya Kiswahili.
  • Item
    Matumizi ya tarakilishi katika ufundishaji wa fasihi simulizi katika shule za upili nchini Kenya: Uchunguzi kifani wa kaunti ya Bungoma
    (Kibabii University, 2018-05) Kibiti, David Barasa
    Matumizi ya teknolojia za kisasa katika mawasiliano ni muhimu sana leo. Katika muktadha wa elimu, mbinu za kurahisisha mawasiliano darasani ni muhimu ili kuhakikisha matokeo mema katika mtihani na pia kuwaandaa wanafunzi katika matumizi ya vifaa vya kisasa wanapomaliza shule. Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu matumizi ya tarakilishi katika shughuli za elimu lakini hapana wowote tulioshuhudia unaohusu ufunzaji wa Fasihi Simulizi kwa kutumia tarakilishi. Pengo hili ndilo ambalo limejenga msingi wa utafiti huu. Basi katika utafiti huu, Mtafiti alichunguza matumizi ya tarakilishi katika ufunzaji wa Fasihi Simulizi. Utafiti huu hasa ulilenga kutathmini ni kwa kiwango kipi walimu wa Kiswahili hutumia tarakilishi katika kufunza Fasihi Simulizi. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Ukubalifu na Utumizi wa Teknolojia iliyoasisiwa na Rogers (2003). Nadharia hii inafafanua hatua wanazopitia watumizi kabla ya kuanza kutumia teknolojia mpya katika shughuli zao. Utafiti uliegemea muundo wa kithamano na mkabala wa usoroveya na ulifanywa katika shule teule za upili katika kaunti ya Bungoma. Sampuli ya shule 18 iliteuliwa katika jumla ya shule teule za kaunti ndogo katika kaunti nzima. Shule hizi zimepandishwa vyeo mwaka wa 2010 na kufanywa kuwa shule teule katika kila eneo bunge. Wasailiwa walipatikana kutoka kwa jumla ya shule 314 za kaunti ya Bungoma. Sampuli ilijumlisha walimu wa Kiswahili 36, walimu wakuu 18 wa shule zilizoteuliwa. Jumla ya watafiti walikuwa 54. Mbinu za kuteua sampuli zilikuwa sampuli maksudi, sampuli nasibu tabakishi na sampuli nasibu. Utafiti huu ulitumia hojaji na mahojiano kama mbinu za kukusanya data. Hatimaye, data hizo zikawasilishwa na kuchanganuliwa kwa majedwali, nambari na asilimia. Mtafiti alipata kwamba shule zote kati ya zilizoteuliwa zina tarakilishi. Hata hivyo, hizi tarakilishi hazikutumiwa na walimu katika shughuli za kufunza darasani. Pia, ilibainika kuwa kuna changamoto zinazoathiri matumizi ya tarakilishi kama wenzo wa kufunzia. Mfano mwema ni ukosefu wa ujuzi wa tarakilishi miongoni mwa walimu na umeme usiotegemewa. Inatarajiwa kwamba matokeo yatawasaidia walimu kuboresha mbinu za ufunzaji hasa wa Fasihi Simulizi kwa kutumia teknolojia za kisasa. Serikali na wadau katika elimu watayaboresha mazingira ya elimu.