Usimulizi wa riwaya ya Nyongo mkalia ini
Abstract
Tukichunguza hazina ya uhakiki uliofanywa katika taaluma ya fasihi ya Kiswahili
na kuiweka katika mizani, upande mmoja ubebe tahakiki zilizozingatia maudhui na
mwingine zile zilizoangaza fani, upande wa maudhui utalemewa na uzito na
kuanguka. Ni kweli kuwa umuhimu wa fasihi katika jamii unatokana na jinsi
ambavyo inaimulika jamii na kuichora kwa madhumuni ya kuihakiki na
kuirekebisha kutokana na udhati na uzito wa mafunzo mwafaka inayoyabeba. Ni
kweli vile vile kuwa fasihi ni sanaa kutokana na matumizi ya pekee ya lugha na
vipengele vingine vya fani ambavyo kwa pamoja huipa sura maalum na kuyafanya
maudhui yake yatufikie katika hali na umbo linalovutia. Hali hii ndiyo huiwezesha
fasihi kutuingia, ikatuchoma na kutufikirisha zaidi. Ndio nguzo ya utamu wa fasihi.
Katika misingi hiyo, uendelezaji wa fasihi; hasa kwa upande wa uhakiki
unapaswa kuzingatia pande zote mbili za sarafu; yaani maudhui na fani
inayoyabeba maudhui hayo. Makala hii imelengwa kutoa mchango huo kwa kuupa
uzito upande wa fani ya fasihi kwa kuzingatia kipengele cha usimulizi. Nao uteuzi
wa usimulizi umechochewa na ukweli kuwa mbinu hii haijachunguzwa na wahakiki
wengi katika fasihi ya Kiswahili. Awali ya kuchambua jinsi ambavyo mbinu hii ya
usimulizi imejitokeza katika riwaya ya Nyongo Mkalia Ini, dhana ya usimulizi
itafafanuliwa na nafasi yake katika fasihi kuwekwa bayana.
Collections
The following license files are associated with this item: